WARATIBU WA PRESS CLUB ONGEZENI KASI KUFUATILIA VITENDO VYA UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU



Waratibu wa Klabu za Waandishi wa habari nchini (Press Clubs) wametakiwa kuongeza jitihada za kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya waandishi wa habari na kuripoti kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waratibu hao jana Jijini Dodoma, Afisa Programu kutoka klabu za waandishi wa habari nchini UTPC, Victor Maleko amesema waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na kukwamisha utendaji wao wa kazi wa kila siku.

Amesema UTPC kwa ushirikiano na shirika la IMS Denmark wameingia mkataba wa kusimamia ukiukwaji wa uhuru wa habari (madhila), ambayo ni moja ya haki za msingi za kidunia na waratibu kwa kuwa ni kiungo kikubwa wanatakiwa kuongeza juhudi za kuripoti matukio hayo ili kuyakomesha.

Maleko amesema ili kufanikisha zoezi hilo UTPC imekuwa ikitoa mafunzo na midahalo mbalimbali ya ulinzi na usalama kwa mwandishi wa habari ikiwemo waratibu kujengewa uwezo wa kufwatilia madhila dhidi ya waandishi wa habari nchini.

“Leo mko hapa kwaajili ya kujengewa uwezo wa namna bora kufuatilia ukiukwaji wa haki za kupata taarifa na uhuru wa habari ikiwemo madhila dhidi ya waandishi wa habari, tunaamini baada ya mafunzo haya mtarudi kazini mkiwa mko vizuri kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadam kwa waandishi wa habari,”amesema.

Akiwasilisha mada kuhusu uhuru wa kujieleza na akitumia uzoefu wake kitaifa, Wakili John Sendodo amesema ili kuweza kutambua haki za msingi za binaadam ni vyema kujua haki za kimataifa na namna nchi zingine zimekuwa zikitekeleza haki hizo.

Pia amesema kumekuwepo na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binaadam ambayo Tanzania ni miongoni mwa mwanachama wake hivyo ni vyema waratibu wakaelewa na kujua mipaka yao wakati wa kuripoti matukio hayo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la IMS Zimbabwe, Rashweat Mukundu ametoa uzoefu wake kuhusu madhila yanayotokea Zimbabwe na kuwataka waratibu hao kuwa makini wakati wa kuchambua madhila hayo kwa kuwa wanaoyafanya na wao hutumia akili nyingi sana.

“Nchini Zimbabwe waandishi wa habari wanafanyiwa sana madhila lakini kama hauko makini unaweza usibaini ukweli wa tukio lililotokea, hivyo mbinu mbalimbali zinahitajika ili kuweza kubaini,”amesema.

Pia amewataka waratibu kuripoti haraka matukio ya madhili pindi yanapotokea ili kurahisisha upatikanaji wa mwandishi aliyetendewa tukio husika lakini pia kufanya uchambuzi wa kina na kubaini ukweli ili kuepuka mgogoro usiokuwa wa lazima na mamlaka za kiserikali.

 

Comments

Popular posts from this blog

Wakulima Rukwa kutumia zana bora kuongeza uzalishaji wa mazao msimu mpya wa kilimo

UTPC KUENDELEA KUELIMISHA UMMA,UMUHIMU WA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

MAENDELEO YA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA