BILIONI 18 KUANZA UJENZI WA BARABARA 3 GEITA


 

BILIONI 18 KUANZA UJENZI WA BARABARA 3 GEITA.

 

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 18 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara tatu mkoani humo.

 

Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.

 

“Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imetenga Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyamirembe hadi Katoke (Km 50), Bilioni 6 kwa ajili ya barabara ya Geita hadi Kahama (Km133), na Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Geita hadi Nzega (Km 54),” amesema Senyamule.

 

Ameongeza kuwa barabara hizo tatu ambazo hadi sasa zimetengewa jumla ya shilingi Bilioni 18, zinaendelea na taratibu za ujenzi, vilevile kwa barabara ya Katoro hadi Ushirombo ambayo iko kwenye mpango wa ujenzi inaendelea kufanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu na inatarajia kupata fedha za ujenzi kutoka Benki ya Dunia.

 

Mkuu wa Mkoa huyo ameitaka TANROADS kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kuhusu sheria ya uzibiti uzito wa magari ili kuondoa changamoto za uharibifu wa barabara unaofanywa na magari yaliyozidisha uzito kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi na ukarabati wa barabara nchini, fedha ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine yenye uhitaji endapo ulinzi wa miundombinu ya barabara nchini utaimarishwa.

 

“Msukumo wa mafunzo haya unatokana na changamoto za mara kwa mara kwa baadhi ya wasafirishaji kutofahamu sababu zinazopelekea gari kukutwa limezidisha uzito katika mizani za TANROADS ambapo katika kituo kilichotangulia gari hilo hilo lilipimwa na halikuwa limezidisha uzito” amefafanua Senyamule.

 

Akisoma taarifa yake kwa Mgeni Rasmi, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Geita, Mhandisi Gladson Yohana, amesema kuwa semina ya mafunzo ya uzibiti uzito wa magari kwa mwaka 2021 ilianza kutolewa mwezi Oktoba katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Njombe, Mbeya, Rukwa, Kigoma na baada ya mkoa wa Geita mafunzo hayo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine iliyobaki ili kuwaongezea uelewa wasafirishaji wengi zaidi.

 

Kwa upande wake, msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Mhandisi Leonard Saukwa, amewaambia waandishi wa habari kuwa Serikali imeweka tozo kwa wanaozidisha uzito wa magari ili kuilinda miundombinu ya barabara nchini, na kuwa gharama za tozo kwa magari yaliyozidisha uzito zinatofautiana kulingana na uzito wa gari husika. Aidha, tozo hizo hubadilika kila baada ya miaka kumi kutokana na mabadiliko ya gharama za matengenezo ya barabara.

 

Nao wadau wa usafirishaji wanao hudhuria mafunzo hayo mkoani Geita, kwa nyakati tofauti wamesema kuwa, kinacholeta mkanganyiko zaidi katika huduma za mizani ni mizani hizo kuwa na majibu tofauti katika upimaji, mizani moja inasoma uzito tofauti na mizani iliyotangulia na kwamba wanaamini kuwa kupitia mafunzo hayo watapata uelewa zaidi kuhusu kutofuatiana kwa vipimo vya uzito baina ya vituo vya mizani .

 

Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018, inatumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilianza kutumika rasmi nchini Tanzania mnamo mwezi Machi mwaka 2019 kwa lengo la kuoanisha viwango vya uzito wa magari ili wafanyabiashara wa nchi hizo waweze kufanya biashara ya usafirishaji kwa utaratibu unaofanana.

 

Imetolewa na, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

 

Comments

Popular posts from this blog

Wakulima Rukwa kutumia zana bora kuongeza uzalishaji wa mazao msimu mpya wa kilimo

UTPC KUENDELEA KUELIMISHA UMMA,UMUHIMU WA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

MAENDELEO YA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA