WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAAGIZWA KUKAMILISHA MAANDALIZI YA CHANJO YA POLIO

 Waganga wakuu wa Mikoa ya Rukwa ,Songwe,Katavi,Mbeya na Kagera wametakiwa kukamilisha maandalizi ya Kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya Polio inayotarajiwa kufanyika tarehe 21 hadi 24 Septemba 2023.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Tumain Nagu ametoa maelekezo hayo Leo tarehe 15 Septemba 2023 alipofanya kikao na watumishi wa sekta ya Afya mkoani Rukwa.

Profesa Nagu ametoa maelekezo kwa waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya zilizomo katika mikoa hiyo kukamilisha maandalizi kabla ya tarehe hizo.

Amesema kuwa polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababisha ulemavu wa viungo na unaoweza kusababisha kifo.Njia mojawapo ya maambukizi ni kupitia kinyesi hivyo ametaka wananchi wote wakumbushwe na kuelekezwa kuwa na vyoo Bora na kuvitumia kwa usahihi.

Amewataka waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka nane kushuka chini anafikiwa pasipo kujali changamoto za kijiografia .

Amewaeleza kuhakikisha chanjo inapatikana katika maeneo yote yaliyotengwa kwa shughuli hiyo na kuhakikisha hamasa kwa wananchi inatolewa kupitia Vyombo vya Habari na kurasa za mitandao ya kijamii.


Mkakati maalumu umewekwa ili kuhakikisha chanjo hiyo inafikia watoto wanaoishi katika maeneo ya mbali  na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa kuwa na timu zitakazotoa huduma tembezi.

Profesa Tumaini Nagu ameyashukuru mashirika ya Kimataifa,ikiwemo Shirika la Afya Duniani(WHO) na UNICEF,kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kutokomeza Polio.

Watoto 391,883 wanatarajiwa kuchanjwa katika Mkoa wa Rukwa.




Comments

Popular posts from this blog

Wakulima Rukwa kutumia zana bora kuongeza uzalishaji wa mazao msimu mpya wa kilimo

UTPC KUENDELEA KUELIMISHA UMMA,UMUHIMU WA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI

MAENDELEO YA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA