PLAN INTERNATIONAL YACHANGIA VIFAA VYA ELIMU RUKWA
Shirika la Plan International Tanzania limekabidhi msaada wa
vitabu, vyoo shirikishi na miundombinu ya maji kwa shule za sekondari na msingi
kwenye Halmashauri za Wilaya Nkasi,
Kalambo na Sumbawanga vyenye thamani ya shilingi Milioni 786 .
Halfa ya makabidhiano ya msaada huo imefanyika katika shule ya
msingi Milundikwa wilaya ya Nkasi jana (Januari 19,2023) ambapo Mkuu wa Wilaya
ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alipokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa Queen Sendiga.
Waryuba akizungumza kwenye hafla hiyo alitoa pongezi kwa
shirika hilo kwa kuchangia vyoo shirikishi 17 na miundombinu ya maji katika shule za
msingi 7 na sekondari 9 katika Wilaya za Nkasi, Sumbawanga Vijijini na Kalambo
vyenye jumla ya thamani ya shilingi za kitanzania 716, 607, 527.
Plan International imetoa pia vitabu vya kiada 10, 128 kwa shule za msingi
29 za wilaya ya Nkasi vyenye thamani ya
shilingi za kitanzania 70, 210, 000
vitakavyotumika kufundishia na kujifunzia wanafunzi na walimu.
“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na
Shirika la Plan International kwa kushirikina na Serikali katika kujenga uwezo
na kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa shule za msingi na awali katika Mkoa
wa Rukwa na kuleta maendeleo ya watanzania katika sekta mbalimbali za kijamii,
alisema Waryuba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Plan International Tanzania Mona Girgis alisema lengo la shirika ni
kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wanafunzi hususan watoto wa kike ndio
maana linashirikiana na serikali kuboresha miundombinu ikiwemo vyoo bora na
safi na vitabu.
Mkurugenzi huyo alisema pia shirika limefanikiwa kutoa mafunzo
ya kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK)
kwa walimu wa darasa la kwanza na la pili wapatao 48 kutoka shule za msingi
22 zilizopo kwenye kata 5 za Nkandasi, Mashete, Mkwamba, Kate na Mtenga wilaya
ya Nkasi.
Kwa upande wake Angela Kayawe ( 14) mwanafunzi wa Darasa la
Saba shule ya msingi Milundikwa alitoa shukrani kwa shirika la Plan International
kwa msaada walioutoa utakaosaidia kuimarisha taaluma mingoni mwa wanafunzi.
Comments
Post a Comment