Bashe akemea vikali wakulima wanaouza namba za
*Bashe akemea vikali wakulima wanaouza namba za siri*
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe leo tarehe 22.11.2022 amewakemea vikali wakulima wanaowauzia wafanyabiashara namba zao za siri kwa ajili ya kupata mbolea za ruzuku kwa njia za udanganyifu.
Mhe.Bashe alizungumza hayo wilayani Kondoa alipopewa nafasi na Mh Rais Samia Hassan Suluhu akiwa ziarani kuelekea Mkoani Manyara.
Waziri Bashe amesema wakati serikali ya Awamu ya Sita inafanya kila jitihada kuwapunguzia wakulima gharama ya mbolea, baadhi yao wanahujumu jitihada hizo.
Akitoa mfano Waziri huyo wa kilimo amesema wakulima wapatao 20 mkoani Kigoma wamekamatwa kwa tuhuma za kuwauzia wafanyabiashara wa mbolea namba zao za siri kwa ajili kupata mbolea za ruzuku.
"Napenda kuwafahanisha wakulima wote nchini kuwa mfumo tunaotumia kutoa mbolea za ruzuku ni wa kidigitali, hivyo chochote kinachofanyika katika mfumo huo tunakifahamu", alisema Bashe.
Amewaonya wote watakaojihusisha na vitendo vya udanganyifu ili kuhujumu mpango wa serikali wa utoaji mbolea za ruzuku kuwa watachukuliwa hatua kali.
Waciri Bashe amewataka wakulima kununua mbolea kwa bei za ruzuku zilizowekwa na serikali ili kuwapunguzia makali ya pembejeo hiyo muhimu.
Akizungumzia kuhusu uuzaji wa mazao, Bashe amesema serikali imetoa ruhusa kwa wakulima kuuza mazao yao mahali popote na kuacha ziada itakayotumika kama chakula.
Amesema kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, mwaka huu kuna mvua kidogo hivyo amewataka wakulima kutumia mvua za kwanza kupandia na kulima mazao yanayostahimili ukame kama vile mihogo na mtama.
Aidha amempongeza Rais Samia kwa utashi wake wa kisiasa wa kuwekeza zaidi kwenye sekta ya Kilimo, ambapo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, wizara yake imepatiwa kiasi cha takribani Tsh. billioni 900
Amesema uwekezaji mkubwa uko katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji ambayo pia itatumika kwa ajili ya kuandaa mbegu za alizeti zitakazotolewa kwa bei ya ruzuku.
Waziri Bashe amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa njaa kwani serikali ina chakula cha kutosha.
" Tayari tumepeleka chakula katika halmashauri 41 ili wananchi wauziwe kwa bei nafuu",
Alisema Bashe.
Comments
Post a Comment