RC SENDIGA: TUTAFANYA MAPINDUZI YA KILIMO RUKWA
RC
SENDIGA: TUTAFANYA MAPINDUZI YA KILIMO
RUKWA
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Queen Sendiga amesema anatamani kuona mkoa wa Rukwa ukifanya mapinduzi makubwa
katika sekta ya kilimo kiwe cha kibiashara na kukuza uchumi wa wananchi.
Ili kufanikisha hilo
amewataka wataalam wa kilimo katika halmashauri zote nne za Rukwa kuja na
mikakati ya kufanya kilimo kichangie zaidi katika kukuza pato la wananchi na
kuongeza uhakika wa chakula.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema
hayo jana mjini Sumbawanga (10 Agosti, 2022) wakati wa hafla rasmi ya
makabidhiano ya ofisi toka kwa mtangulizi wake Joseph Mkirikiti kufuatia Rais
Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
“Natamani kuiona Rukwa
ikifanya mapinduzi makubwa katika kilimo. Maafisa kilimo na ugani jitahidini kuwa
na mipango mizuri ili kilimo chetu kiwe cha kibiashara na kuhusisha vijana
wengi “alisema Sendiga.
Sendiga aliongeza kusema
mkoa lazima uwe na mkakati wa kufanya vijana wengi kurudi vijijini ili kufanya
kazi za kilimo hatua itakayowapatia uhakika wa ajira hivyo kutimiza lengo la Rais
Samia kutaka kuona kilimo kuzalisha ajira nyingi nchini.
Katika hatua nyingine
Sendiga amewaeleza wananchi kuwa atapenda kuona mkoa wa Rukwa ukipiga hatua
kubwa katika sekta ya elimu ili watoto wengi zaidi wafaulu mitihani na taaluma
kukua zaidi.
Kuhusu usimamizi wa mapato
na matumizi ya fedha za umma, Sendiga ametoa rai kwa halmashauri za Rukwa
kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ili fedha nyingi zaidi zitumike
kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Natamani wataalam wa halmashauri
waje na mipango madhubuti ya ili tuwe na miradi inayokamilika kwa wakati
.Sipendi kuona maboma yasiyokamilika kwenye halmashauri zetu” alisisitiza
Sendiga.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa anayemaliza muda wake Joseph Mkirikiti alitumia nafasi hiyo kuwaaga wana
Rukwa ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini kipindi
alichoongoza mkoa huo.
Naye Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala akizungumza kwenye hafla hiyo alimpongeza Mkuu wa
Mkoa mpya ambapo alimtaka kushirikiana na chama hicho kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi.
“Tunaamini kazi unayokuja
kufanya Mkuu wetu mpya wa Mkoa (Sendiga) ni usimamizi wa utekelezaji wa Ilani
ya CCM ili wananchi wa Rukwa wapate maendeleo. Tuko tayari kushirikiana nawe”
alisema Lukala.
Lukala aliongeza kusema wanampongeza
Mkuu wa Mkoa aliyepita Joseph Mkirikiti kwa ushirikiano wake na chama na kuwa
wamepokea mabadiliko yaliyofanywa na Rais vema.
Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga
anakuwa mkuu wa mkoa wa Rukwa wa 17 tangu ulipoanzishwa mwaka 1974.
Mwisho.
Comments
Post a Comment