MAENDELEO YA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA

 

CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA CHAFIKIA 64% KUJENGWA


Na. OMM Rukwa


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuwezesha upatikanaji  fedha shilingi 3,852,697,911 zinazotumika katika awamu ya kwanza kujenga majengo 11 ya chuo kipya cha Ualimu Sumbawanga eneo la Pito ambapo mradi huo umefikia asilimia 64 hadi sasa.


Akizungumza leo (06. 07.2022) kwenye ukaguzi wa mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwaeleza waandishi wa habari kuwa serikali inatekeleza mradi huo kwa lengo la kufungua fursa za kielimu kwa wananchi ambapo utakapokamilika utasidia kuchochea ukuaji wa uchumi.


"Rukwa tumenufaika na mradi huu wenye thamani ya shilingi Bilioni 3.9 ambapo majengo kadhaa yamekamikika na mengine jitihada za ukamilishaji zinaendelea vizuri. Nimeridhishwa na  kazi inayoendelea hapa na kuhusu changamoto chace nitawasiliana na Wizara ya Elimu tuzitatue mapema na mradi ufike mwisho" ,alisema Mkirikiti. 


Katika hatua nyingine Mkuuu huyo wa Mkoa alipongeza Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoani humo kwa kazi nzuri iliyofanya na inayoendelea kuifanya kufuatilia mwenendo wa matumizi ya fedha za umma hatua iliyosaidia mradi wa chuo hicho kutekelezwa vizuri.


Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mhandisi  Mshauri  toka Chuo cha Ufundi Arusha Emanuel Didas alisema mradi umefikia asilimia 64 za ujenzi ambapo jumla ya shilingi Bilioni 2.5 kati ya shilingi Bilioni 3.0 zilizopokelewa mwezi Mei mwaka huu zimetumika hadi sasa.


Mhandisi Didas alisema jumla ya majengo 11 yamejengwa na yapo katika hatua za ukamilishaji ikiwemo jengo la madarasa lenye vyumba 8, mabweni mawili yenye uwezo wa wanafunzi 250 kila moja, vyoo vya nje, nyumba za watumishi ,jiko na bwalo na vibanda vya walinzi.


Mradi wa ujenzi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga awamu ya kwanza kupitia mradi wa Education Program for Resultfs (EP4R) chini ya Wizara ya Elimu ulianza 15 Agosti 2021 na unatarajia kukamilika Julai mwaka huu. Kwa sasa chuo kinatumia majengo ya Kanisa Katoliki eneo la Kantalamba kwa ajili ya mafunzo.


Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

Watumishi Wa Umma Wilayani Kalambo Waungana Kuadhimisha Kumbukizi Ya Mashujaa Kwa Kufanya Usafi.

Dc Kalambo Ataka Walio Husika Kumuozesha Mwanafunzi Wa Darasa La Saba Kukamatwa

Mkurugenzi UTPC awataka Waandishi kuandika Habari za Usawa wa kijinsia ili kuleta mabadiliko Chanya katika jamii.