Ahukumiwa Mwaka Mmoja Na Nusu Kwa Kosa La Wizi
Na baraka Lusajo - Rukwa
Mahakama ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imemuhukumu kwenda jela mwaka mmoja na nusu Frank Geoffrey Sikazwe (28) mkazi wa kijiji cha Kasanga wilayani humo kwa kosa la wizi.
Mtuhumiwa alishitakiwa kwa makosa mawili baada
ya kuvunja nyumba ya Lauriano Simbeye huko
Kasanga usiku wa tarehe 05 Februari 2020, akiwa na kusudio la kuiba kinyume na
kifungu 294(1)(a) and (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya
mwaka 2019, pia kosa la wizi kinyume na kifungu 258(1)(2)(a) na 265 cha sheria
ya kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya mwaka 2019.
Mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Matai na kuandaliwa hati ya mashitaka hatimaye kufikishwa mahakamani. Baada ya kusomewa mashitaka alikana kutenda kosa hilo suala lililopelekea upande wa mashitaka kuwa na jukumu la kuthibitisha pasi na shaka tuhuma zinazomkabili mshitakiwa.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu wa mahakama ya
wilaya ya Kalambo Ramadhani Rugemalira, alisema
mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa kwa makosa hayo baada ya kujiridhisha na
ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Mwendesha mashitaka kwa upande wake hakuwa na kumbukumbu za nyuma za mshitakiwa lakini aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kwa kuwa vitendo hivyo vimekithiri katika jamii.
Comments
Post a Comment